Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Wizara ya Ulinzi ya Afghanistan imetangaza kwamba, wanachama 11 wa kundi la Taleban waliuawa katika mapigano yaliyojiri katika viunga vya mji wa Kunduz, kaskazini mwa nchi hiyo, huku watu wanane wengine wakijeruhiwa. Kadhalika jeshi la serikali ya Afghanistan limefanikiwa kusambaratisha shambulizi la wanachama wa Taleban katika mji huo wa Kunduz. Aidha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Afghanistan imetangaza habari ya kuuawa wanachama 15 wa kundi hilo katika mapigano na maafisa wa jeshi la serikali katika jimbo la Logar, Zabul na Herat.
Katika upande mwingine wanachama wa Taleban waliopenyeza kati ya polisi katika moja ya vituo vya jimbo la Kunduz, wametekeleza shambulizi ambalo limeua polisi watano na wengine saba kujeruhiwa. Khalil Asir, Msemaji wa Jeshi la Polisi katika jimbo la Takhar amesema kuwa, watu sita miongoni mwa wapiganaji wanaoiunga mkono serikali ya nchi hiyo wameuawa katika shambulizi lililotekelezwa na wanachama wa Taleban katika mji wa Baharak, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Aidha Hanif Rezai, msemaji wa kamandi ya jeshi kaskazini mwa Afghanistan amenukuliwa akisema kuwa, jumla ya wanachama tisa wa kundi la Taleban wameuawa katika shambulizi la anga lililotekelezwa na jeshi katika ngome ya wanachama wa kundi hilo katika mji wa Qush Tappeh wa jimbo la Jowzjan.